Sunday, October 7, 2012

Mahusiano:‘Ngoja nipumzike, sitaki, nimechoka’ huharibu mapenzi


MAISHA ya ndoa ni mazuri, lakini ni suala la msingi sana kuwa makini na ulimi pamoja na matendo yetu.
Kimsingi ni kwamba huwa ni kitu cha kusikitisha kidogo, mtu anaingia kwenye uwanja kwa ajili ya kucheza mpira kwa mfano, halafu hachezi amesimama tu kama mlingoti!
Unapoingia kwenye ndoa, pamoja na mambo mengine unapaswa kuwa makini na matendo ambayo unamwambia mwenzi wako.
Unapoingia kwenye ndoa unatakiwa kuwa tayari na yale ambayo hufanyika kwenye ndoa. Ni makosa kuingia kwenye ndoa, halafu unakuwa mwanandoa kero, kila kitu unachoambiwa wewe jibu ‘mimi siwezi, aaah nimechoka, sitaki, jana nimekupa na leo unataka tena, kwani mimi ng’ombe, aaah hata ng’ombe huwa anachoka vilevile’.
Kutwa nzima watu wamekuwa wakihangaika na maisha, inatia hasira unarudi nyumbani nako ni shida nyingine inatokea, ukifanya hiki, sitaki, nimechoka, naumwa kichwa, aaah subiri kwanza nipumzike’
Wenye kauli kama hizi wengi ni wanawake, ingawa pia wapo wanaume wachache. Kama ni wanaume basi huenda kuna kasoro, labda mwanaume anaanza kuwa na dalili za matatizo ya uwezo wake wa kiume, anaumwa magonjwa fulani hasa kama nyumba ya mgongo kwa chini kuna maumivu na wakati mwingine ni dalili za upendo kupungua.
Kwa asilimia kubwa wanaume huwa hawachoki kiasi cha kusema sitaki au siwezi. Akisema hivi basi ni dalili kama hizo za juu. Hata hivyo hata kama mwanaume anasumbuliwa na tatizo la nguvu, kuna vyakula ambavyo anaweza kula na hali yake inaweza kuwa nzuri, kama ambavyo mara kadhaa nimewahi kueleza katika makala zangu.
Wengine wanasumbuliwa na tatizo hili la nguvu, kwa sababu walifanya sana michezo kama ya kujichua, kulewa, kutumia dawa za kulevya, kufanya mazoezi sana kisha kuacha, kuvuta sigara, kutumia dawa za magonjwa hasa ya kisukari, moyo (baadhi ya dawa husababisha nguvu kupungua). Hata hivyo kwa vyovyote itakavyokuwa tiba yake ipo kama nilivyoeleza hapo juu, huna sababu ya kuwaza mabaya au kukata tamaa. Kukata tamaa katika maisha ni kosa kubwa.
Ndugu yangu natamani siku moja usiku Mungu angefungua mapaa yote ya nyumba wanazolala wanandoa halafu uone namna wengi wao wanavyolala, bila shaka kama bado hauko kwenye ndoa, usingeshawishika siku moja uwe mwanandoa.
Ninachotaka kusema ni kuwa ndoa nyingi zimejaa maigizo, watu wanaishi wanacheka, wengi wao wanaishi tu kwa shida, hakuna maelewano ya kutosha. Ndoa yako ikoje?
Baadhi ya nyumba kwa mfano, unaweza kuona mmoja anamlalamikia mwingine kwa kutokuwa mwaminifu nk. Baadhi ya nyumba pia utaona watu wamelala sebuleni, mmhh baba mzima au mama mzima ambaye unamuona mitaani, yanayoendelea kwenye nyumba yake ni vigumu kuamini kama kweli huyu fulani anaweza kufanya.
Msingi wa yote haya ni sisi wenyewe namna ambavyo tunatumia ulimi na matendo yetu, hivyo ni muhimu kuwa makini.
“Ngoja nipumzike, sitaki, aaah nimechoka”, ni kati ya kauli ambazo zinaharibu mapenzi. Je, wewe umewahi kuzitumia? Ni vizuri kuachana nazo. Umeingia kwenye mpira uko katikati, ni vizuri kuangalia namna ya kuucheza badala ya kuleteana kero ndani ya ndoa.
Mapenzi kama mnakomoana
Hekima pia inahitajika kujua mwenzangu yukoje na nifanyeje ili kwendana naye, maana kuna wengine kila siku anataka, kwa baadhi ya wanandoa huwa hawataki sana hilo, anaona kama unamkomoa. Kwa wiki angalau siku tatu si mbaya.
Hakuna athari za kisaikolojia za kukutana mara kwa mara kama wenyewe mnapenda, lakini si mbaya pia kubuni mbinu zingine za kukutana ili kuboresha uhusiano wenu na kufurahiana zaidi, japo tafiti nyingi zinaonyesha kuwa tendo linapofanywa mara nyingi linasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha ndoa na kuwafanya wanandoa kupendana sana, kuliko wale ambao akiguswa aaah sitaki, jana nimekupa na leo unataka’.
Lakini pia mwenzi wako anapotaka, si hekima kusema sitaki, badala yake unapaswa kumsaidia kutimiza anachotaka, ziko njia nyingi hata kama ni kucheza tu, si ndio jamani?  
Mapenzi ni zaidi ya ‘kupigana ugomvi wa baba na mama’, mnapaswa kwa mfano kuwa mnatembea pamoja, kula pamoja, kuoga pamoja, kuzungumza kauli nzuri na mambo kama haya.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment