Tuesday, September 25, 2012

Mke wangu ana kadi mbili za kliniki, moja jina langu, lingine la bwana mwingine!


Mpenzi msomaji, usione watu wanaangua vicheko barabarani na wakati mwingine hadi machozi yanawamwagika.
Ni kweli kwamba yapo machozi ya furaha lakini pia machozi mengine ni uchungu unaoonekana kama aina fulani ya furaha. Upo mpaka hapo msomaji wangu?
Mtu anaweza kucheka lakini siyo kweli anacheka kutoka moyoni bali anajaribu kuficha yanayomkera lakini katika kujipa moyo anashiriki kicheko pale anapozungumza na jamaa au rafiki yake.Huo ni ukweli.
Ushiriki huu wa kicheko, hakika humpunguzia mawazo fulani kwani vile nijuavyo mimi kicheko ni afya. Hufanya hata makunyanzi kwenye uso kupotea kwa muda.
Lakini pia kipo kicheko cha ukweli kinachotokana na jambo fulani la kufurahisha alilokujulisha mwenzako na katika kuonyesha wingi wa furaha, chozi nalo hujikuta likimwagika. Je, imewahi kukutokea hivyo msomaji wangu? Mimi Yes!mara nyingi tu.
Naam.Nimeanza hivyo ili kukuweka sawa kwa kile tutakachojadili hapa chini kwamba usione watu wanapita barabarani, wako maofisini wakichapa kazi ukadhani wana furaha tele moyoni.
Pale kazini wanajitahidi au niseme wanajitutumua tu kutimiza wajibu lakini baadhi wanapofikiria kule majumbani wanakotoka, mapigo ya moyo huenda mbio na afadhali kama angeambiwa apige mbio lakini yanamdunda wakati katulia tuli. Kisa amekumbuka vitimbi vya nyumbani kwake. Hebu msikie kijana huyu, kisha umpe ushauri na uchangie mada nini kifanyike
Yupo msomaji mzuri wa safu hii amenitumia ujumbe mfupi kwenye e-mail ya safu hii akieleza machungu yake ndani ya ndoa na kujikuta njia panda. Anaanza namna hii:
“Habari Ant, pole na kazi kubwa uliyonayo hususani hii ya kutoa ushauri kwa watu wenye shida kama sisi.
Mara nyingi nimekuwa nikifuatilia mada zako unazotoa kwenye hili gazeti pendwa la Nipashe Jumapili kwa njia ya mtandao wa intaneti.
Kusema ukweli kila ninaposoma ushauri wako unaowashauri watu wenye shida huwa nafarijika sana na ndio kitu kilichonifanya na mimi nitoe dukuduku langu linalonisumbua kichwa changu kiasi kwamba hapa niko njia panda sijui nielekee wapi.
Naanza hivi: Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 28, nimejaliwa kufunga ndoa na mke wangu miaka 3 iliyopita, ingawa tumechelewa kupata mtoto lakini ndoa yetu ina upendo na amani.
Mwezi wa Machi mwaka huu, mke wangu alifanikiwa kupata ujauzito kitu ambacho kimeongeza upendo ndani ya nyumba yetu na mimi najitahidi kadri ya uwezo wangu kuhakikisha mke wangu anapata mahitaji yake yote muhimu kiasi kwamba hakuna kitu anachokikosa.
Hata hivyo, kilichonifanya niombe ushauri kutoka kwako na wadau wote kwa ujumla, ni kwamba hivi karibuni nimemfuma mke wangu kwenye kabati lake la nguo nimekuta ana kadi mbili za kliniki, moja ina jina langu na ya pili ina jina la bwana mwingine hizo kadi zote kaziandikisha vituo tofauti.
Kwa kweli baada ya kuzifuma kadi hizo nilichokifanya nilizirudisha nilipozikuta na mpaka hivi sasa mke wangu hajui chochote kinachoendelea.
Ndugu wadau wa safu hii mwenzenu yamenikuta nimebaki njia panda kiasi kwamba nashindwa la kufanya. Naombeni ushauri wenu kabla sijachukua uamuzi wowote. Nawakilisha”.(Msomaji Dar).
Mpenzi msomaji, bila shaka umemsikia vema mwenzetu katika balaa lililomkuta. Ni mke lakini anamficha jambo kubwa kama hilo. Angalia Mungu alivyo mwema, kamwelekeza hadi akaziona kadi zile kumdhihirishia kuwa mke yule siyo mwaminifu lipo jambo anamficha.
Kinachoonekana dhahiri ni kwamba mke huyo ana Mashaka na nani hasa baba wa mtoto wake kwani yawezekana kutokana na kukaa muda mrefu bila kupata ujauzito ndani ya ndoa, iko siku alitoka nje ya ndoa na kupata ujauzito.
Sasa anajaribu kujihami ili kama mtoto atafanana na baba mtoto wake wa ndoa iwe heri. La kama atafanana na yule wan je ya ndoa basi bomu likifumuka ajue pa kuegemea.
Uaminifu ukiwekwa kando ndio mambo kama hayo huweza kujitokeza na hili limeleta shida sana katika nyingi ya nyumba zetu. Mtu anaona raha kutoka nje ya ndoa lakini yakimfika ya kumfika ndio kama hivyo anaanza kutapatapa na kufungua kadi mbili kliniki tofauti.
Wapo baadhi ya wanawake ambao baada ya kugundua amepata ujauzito na mwanaume wan je, ili kufuta ushahidi huamua kutoa mimba hiyo. Haya ni mauaji ambayo hayawezi kusameheka mbele za Mungu.
Na yote haya yanatokea kutokana na uaminifu kupungua sana ndani ya familia zetu. Msomaji wangu hebu changia maoni katika jambo hilo.
Kwa hitimamisha makala haya, hebu nikupe maoni ya baadhi ya wasomaji wetu kuhusu mada iliyopita kuhusu “Bajeti kubwa za kuoa au kuolewa zina tija gani kwa Mtanzania?”.
Mmoja anasema;“kiukweli Aunty ile mada ya Jumapili kuhusu michango ya harusi imenigusa sana kwa sababu mimi binafsi nilifikia kutaka kutengwa na baadhi ya ndugu eti kisa sijamchangia kaka yangu sh. Laki moja na nusu iliyokuwa inahitajika.
Kiukweli niliumia sana na sitanii Aunty nilifichwa hadi tarehe ya harusi…sasa baada ya miezi miwili mke wa kaka akawa anaumwa. Nimeshangaa hatukuona mtu yoyote kati ya wale waliokuwa na sifa ya kutunza siku ya harusi. Kiukweli inabidi tubadilike tujaliane kipindi cha shida na raha.(Salimu wa Dar 0753885140).
Mwingine anasema; nashangaa mie mambo ya siku hizi. Michango mikubwa inatumika kwa siku moja wakati walao robo wangepewa watoto yatima au wagonjwa mahospitalini mbona ingekuwa sadaka toshawanandoa.
Mfano mchango umepatikana milioni 200, unatoa milioni 50 unanunua vyakula unawapatia yatima ndoa zingedumu kutokana na dua/sala kwa yatima.
Mbona wenzetu Wakenya wanachangia matibabu, elimu. Ndoa ni wanandoa tu na zinadumu. Mie naona ni kufuru kwa Mungu kuchezea fedha kwa siku moja wakati watoto yatima wanaongezeka.(Mama Lulu, Kitunda).
Mwingine anasema; huyu anayelalamika haendi katika shughuli za ndugu wala marafiki maana michango unawekeza na siyo lazima uchange zile harusi za kiwango ni cha wanandugu au marafiki wa karibu. Mimi nimeanza kuchanga tangu 1982, nimeozesha 2011 lengo likiwa ni mil.12/- lakini nilipata mil.22/-. Hii ni kwa vile najitoa kwa watu na kiwango kikiwekwa na kama kimati kiwango cha chini ni sh.70,000.
Huyu ndugu hajichanganyi maana shughuli ni watu na watu ndio shughuli(Usitaje namba yangu tafadhali).
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment